Nyong’o atoa wito wa umoja ODM

Martin Mwanje
1 Min Read
Prof. Anyang' Nyong'o - Gavana wa Kisumu

Pande zinazozozana katika chama chama cha ODM zimetakiwa kutuliza joto la siasa linalopanda chamani na badala yake kusuluhisha tofauti kati yao kwa amani. 

Aidha, Gavana wa Kisumu Prof. Anyang’ Nyong’o ameutaka uongozi wa chama kukoma kurushaiana cheche za maneno na badala yake kuheshimiana licha ya kukithiri kwa mivutano chamani.

“Kama mwanzilishi na Katibu Mkuu mwasisi wa ODM; mwangalizi wa sera na kanuni, natoa wito wa umoja na heshima ndani ya uongozi wa chama,” Prof. Nyong’o alisihi.

“Uongozi na wanachama sharti wasalie imara katika maadili yetu muhimu ya demokrasia, ujumuishaji na haki ya jamii kwa watu.”

Wito wake unakuja wakati ambapo mirengo miwili imeibuka chamani, mmoja ukiongozwa na kaimu kiongozi wa chama Dkt. Oburu Oginga huku mwingine ukiongozwa na Katibu Mkuu wa chama aliyetimuliwa kwenye wadhifa huo Edwin Sifuna.

Hata hivyo, Sifuna ambaye pia ni Seneta wa Nairobi ameelekea mahakamani kupinga kutimuliwa kwake.

Kwa sasa, kila upande unavuta kamba upande wake huku mmoja ukitaka chama cha Chungwa kufanya kazi na utawala wa Kenya Kwanza kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 wakati mwingine ukipinga vikali jitihada hizo.

Share This Article