Mwigizaji Nyce Wanjeri na mume wake Leting wanaendelea kushukuru wakenya ambao wamewaonyesha upendo na kuwapa usaidizi wakati huu ambao wanapitia changamoto.
Kupitia Instagram, wanandoa hao wawili wameshukuru kila mmoja aliyewatumia ujumbe wa heri njema na waliowatumia pesa pia.
Wawili hao walichapisha video ya pamoja iliyowaonyesha wakiwa kwenye gari ambapo walisema kwamba wanaelekea kwenye shule ya binti yao mkubwa aitwaye Tasha na kwamba wanamrejesha shuleni.
Tasha alikuwa amekosa kwenda shuleni tangu muhula wa pili kutokana na ukosefu wa karo baada ya wazazi wake kukosa uwezo wa kifedha.
Jana Wanjeri alichapisha video aliyorekodi mwezi Agosti wakati mali yao ya nyumba ilikuwa inatwaliwa kwa ajili ya kupigwa mnada baada ya kukosa kulipa kodi kwa miezi kadhaa.
Katika video hiyo, Wanjeri ambaye ni mama wa watoto wawili alielezea kwamba wamekuwa wakijituma kikazi kama kawaida lakini mambo hayajakuwa mazuri.
Leting kwenye video ya leo alifichua kwamba waliamua kuchapisha video hiyo ya Agosti kwani walikuwa na mahitaji na sasa wamepata usaidizi.
Mwanamuziki huyo amesema kwamba amejifunza kuzungumza kila anapokuwa na shida huku akihimiza wakenya pia kufanya hivyo.
