Mwanamuziki wa kike wa Uganda Winnie Nwagi ametaja mwaka 2026 kuwa mwaka mzuri kwake kuhusiana na kazi zake za muziki.
Akizungumza kwenye mahojiano, mrembo huyo alisema alipata kazi nyingi na ratiba yake ikawa imejaa matukio ya utumbuizaji ikilinganishwa na miaka mingine ya awali.
Nyota huyo ambaye amesajiliwa na kamouni ya muziki ya Swangz Avenue, alisema kwamba mwaka huu umekuwa wenye mafanikio na kumshukuru Mungu kwa fursa alizopata pamoja na hatua aliyopiga katika safari yake ya muziki.
Nwagi alisema mwaka huu umekuwa tofauti na mwaka uliopita, akibainisha kuwa kupata nafasi nyingi za kutumbuiza na kuimba kumemsaidia kusogea karibu na malengo yake.
Aliongeza kuwa hata usimamizi wake wa muziki, kampuni ya Swangz Avenue, umekuwa na shughuli nyingi mwaka huu, akisema hakuna upande unaolalamikia mwenendo wa mwaka huo.
Wakati huo huo, Nwagi amezungumzia urafiki wake na mwimbaji mwenzake Sheebah Karungi, kufuatia maswali kuhusu namna anavyodumisha uhusiano mzuri na Sheebah na Spice Diana, ambao wanaaminika kutokuwa na maelewano mazuri.
Nwagi alisema hana upande anaounga mkono katika tofauti zao na kusisitiza kuwa yeye na Sheebah bado ni marafiki wazuri licha ya kutokutana mara kwa mara kutokana na shughuli nyingi na kuishi maeneo tofauti.
Alisema kila wanapopata nafasi ya kukutana, huwa wanafurahia kuwa pamoja, akibainisha kuwa wote hawana tabia ya kuzunguka-zunguka bila sababu.