Daniel Noboa ndiye mshindi katika kinyang’anyiro cha urais nchini Ecuador ambapo amemshinda Luisa Gonzalez, rafiki wa karibu wa mtoro Rafael Correa ambaye alikuwa rais.
Noboa wa umri wa miaka 35 alitangaza ushindi wake katika mkutano na wanahabari mjini Olon, akisema alikuwa aanze kazi kama Rais mara moja.
“Kesho tunaanza kazi ya Ecuador mpya, tunaanza kujenga upya nchi ambayo imekabiliwa na vurugu, ufisadi na chuki.” alisema Noboa.
Uchaguzi uliandaliwa nchini Ecuador Agosti 20, 2023 kuchagua Rais na wabunge lakini uchaguzi wa urais ukaingia duru ya pili baada ya wawaniaji wote kukosa kutimiza kiwango hitajika cha kura.
Duru ya pili iliandaliwa Jumapili Oktoba 15, 2023 kura zinasemekana kuendelea kuhesabiwa na tayari Noboa amedai ushindi kwa kutumia hesabu ya hadi sasa ambapo asilimia 95 ya kura zote zilizopigwa zimehesabiwa.
Anaongoza kwa asilimia 52.10 huku mpinzani wake Luisa González akiwa na asilimia 47.90.
Noboa amekuwa akifanya kazi katika biashara ya babake mzazi ya ndizi kabla ya kuingilia siasa na aliwashangaza wengi alipoingia kwenye duru ya pili ya uchaguzi wa Urais na sasa atakuwa rais wa umri mdogo zaidi wa nchi hiyo ya Ecuador.
Kwenye kampeni aliahidi kuimarisha uchumi unaodorora wa Ecuador na kuhakikisha uwepo wa fursa za ajira.
Iwapo angeshinda kwenye uchaguzi huu, Luisa Gonzalez, angekuwa rais wa kwanza wa kike wa Ecuador.
Katika kampeni yake aliahidi huduma za bure za afya kwa wananchi na kulinda haki za wafanyakazi vitu ambavyo vilisikika sana wakati wa uongozi wa rafiki yake Correa kabla hajakwenda mafichoni baada ya kukabiliwa na mashtaka ya ufisadi.