Kampuni ya reli ya Ufaransa, SNCF inasema abiria 800,000 wameathiriwa na kile Waziri Mkuu wa nchi hiyo Gabriel Attal alichotaja kuwa “vitendo vya hujuma”.
Kumetokea msururu wa moto uliosababisha usumbufu mapema Ijumaa asubuhi, saa chache kabla ya sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Paris.
Laini kadhaa za treni za mwendokasi za TGV zimeondolewa upande wa magharibi, kaskazini na mashariki mwa mji mkuu na SNCF imeonya kuwa usumbufu huo unaweza kudumu kwa siku kadhaa. Eurostar pia imewaonya wateja kuhusu muda mrefu wa safari na kufutwa.
Hakuna aliyedai kuhusika na Attal alisema kuwa vikosi vya usalama vinawasaka waliohusika.
Ofisi ya mwendesha mashtaka wa umma pia inachunguza tukio hilo.