Njengere: Matokeo ya KCPE katika mtandao wa KNEC ni sahihi

Tom Mathinji
2 Min Read
Afisa Mkuu mtendaji wa KNEC Dkt. David Njengere.

Baraza la kitaifa la mtihani hapa nchini-KNEC, limezungumzia dosari zilizoibuliwa na baadhi ya watahiniwa kuhusiana na matokeo ya hivi punde ya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane-KCPE wa mwaka 2023.

Kwenye taarifa, afisa mkuu mtendaji wa KNEC Dkt. David Njengere, alisema kwamba baraza hilo limepokea malalamishi kuhusu kasoro kwenye matokeo yaliyotolewa kupitia namba ya arafa 40054 iliyotolewa na wizara ya elimu.

Baraza hilo limesema limefahamishwa kwamba matokeo ya baadhi ya watahiniwa yalikuwa yamepangwa vibaya alama na gredi za somo la Kiswahili kwani zilikuwa zimewekwa katika lugha ya ishara.

Dkt. Njengere alisema pia kuna visa ambapo alama za somo la sayansi na masuala ya kijamii na elimu ya kidini, ziliorodheshwa vibaya na zilikosa alama za (+) na (-) kama ilivyotarajiwa.

Dkt. Njengere alifafanua kuwa makosa hayo yaliathiri tu matokeo ya arafa fupi kwani matokeo katika mtandao wa KNEC ni sahihi.

Hata hivyo aliwahakikishia watahiniwa hao kuwa baraza hilo limewasilisha suala hilo kwa mhudumu wa arafa hiyo, na makosa hayo yalirekebishwa ifaavyo.

Mkuu huyo wa KNEC alisema baraza hilo lilipokea zaidi malalamishi kutoka kwa watahiniwa waliopata alama za chini katika baadhi ya masomo, hasa katika masomo ya kiingereza na kiswahili.

Baraza la KNEC limekagua malalamishi yote na kubaini kuwa kulikuwa na watahiniwa 133 walioathirika.

Share This Article