Njambi Koikai afariki

Kevin Karunjira
2 Min Read

Mtangazaji na mpiga muziki Njambi Koikai ameaga dunia. Koikai anaripotiwa kukata roho Jumatatu saa tatu usiku katika hospitali ya Nairobi ambapo alikuwa anapokea matibabu.

Kabla ya hapo, mpenzi huyo wa muziki wa Reggae alikuwa amechapisha ombi la damu akielezea kwamba amelazwa hospitalini na anahitaji damu aina ya O+.

Koikai ambaye aliwahi kufanya kazi na shirika la utangazaji nchini KBC kwenye Metro Fm, KBC Channel 1 na Venus Fm, amekuwa akipambana na ugonjwa wa Endometriosis.

Ugonjwa huo unahusisha kumea kwa seli ambazo zinastahili kuwa kwenye mfuko wa uzazi kwenye sehemu zingine za mwili. Wakati wa hedhi, seli hizo hutoka pamoja na damu na kwa wagonjwa wa Endometriosis, uchungu huwa maradufu.

Wakati alitoa ombi kwa Rais William Ruto kuzuru kituo cha matibabu ya ugonjwa huo nchini Marekani wakati wa ziara yake, Njambi alifichua kwamba ilichukua miaka 17 kabla yake kufahamu alichokuwa akiugua.

Alisema kwamba seli hizo zilisambaa na kufunika mapafu yake kabisa na hivyo kuyafanya kukosa kufanya kazi kila mwezi wakati wa hedhi. baadaye ugonjwa huo uliathiri meno yake, moyo na kidole tumbo au appendix.

Kando na utangazaji kwenye redio ambapo alikuwa akipiga muziki aina ya Reggae na usomaji habari kwa lugha ya kiingereza kwenye runinga, Njambi pia alikuwa anajihusisha na maandalizi ya tamasha za muziki wa Reggae.

Share This Article