Maafisa wa Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS kutoka kituo cha polisi cha KPS Runyenjes na DCI Embu Mashariki walivamia makazi yaliyopo katika kijiji cha Kajekeru na kupata kundi la wanaume wakichinja punda.
Baada ya kufumaniwa, NPS inasema wanaume hao waliojihami kwa silaha butu walijaribu kuwashambulia maafisa hao na kuwalazimu kufyatua risasi hewani kuwatia baridi.
Katika eneo la tukio, mizoga 20 ya punda waliokuwa ndio tu wamechinjwa pamoja na gari aina ya Noah, nambari za usajili KDD 782T vilipatikana.
Bidhaa zingine zilizopatikana wakati wa uvamizi huo ni panga 3, visu 12, upinde 1 na mishale 6.
Watu watatu ambao majina yao ni STANLEY THURANIRA mwenye umri wa miaka 25; GEORGE MARINGA mwenye umri wa miaka 28; na ANASTASIA WANYAGA pia walikamatwa.
Huduma ya Taifa ya Polisi imeupongeza umma kwa kuzidi kutoa taarifa zinazosaidia kukomesha visa kama hivyo.