Katibu mteule wa Utangazaji na Mawasiliano Stephen Isaboke, ameahidi kulinda uhuru wa vyombo vya habari iwapo bunge la taifa, litaidhinisha uteuzi wake.
Alipofika mbele ya kamati ya bunge kuhusu Mawasiliano, Habari na Uvumbuzi leo Ijumaa, Isaboke alisema atashauriana na vyombo vya habari kutatua mizozo kati ya serikali na vyombo vya habari iwapo vitakuwepo.
Alitupilia mbali hatua yoyote ya kukandamiza vyombo vya habari, akitaja hatua hiyo kuwa iliyopitwa na wakati.
“Iwapo kutakuwa na mtafaruku kati ya vyombo vya habari na asasi nyingine, hatua ya kwanza ni mashauriano. Kufunga vyombo vya habari sio mbinu ya kisasa. Hata nyumbani, huwezi wakandamiza watoto wako,” alisema Isaboke.
Isaboke alisema atajizatiti kufanyia marekebisho sheria ya Shirika la Utangazaji nchini KBC na ile ya Habari na Mawasiliano, kuhakikisha sheria hizo ni za kisasa hasaa katika enzi hii ya kidijitali.
Aidha aliahidi kutekeleza mpango wa kufanyia mabadiliko Shirika la Utangazaji nchini KBC, kwa lengo la kulipa madeni yake na kutekeleza mbinu za kuletea shirika hilo mapato.
Isaboke alidokeza kuwa huku serikali ikiendelea kukumbwa na mzigo mzito wa kufadhili KBC, shirika hilo linapaswa kutafuta mbinu za kujihimili kifedha.