Rais William Ruto amewaahidi wakazi wa eneo la Mlima Kenya kwamba, serikali yake itatekeleza na kukamilisha miradi yote katika eneo hilo.
Huku akiondolea mbali hofu kuwa, huenda baadhi ya miradi itakwama, kiongozi wa taifa alidokeza kuwa kufikia mwaka 2027, miradi yote aliyoahidi kutekeleza katika eneo hilo itakuwa imekamilika.
Katika mahojiano na wanahabari kwenye Ikulu ndogo ya Sagana kaunti ya Nyeri Jumatatu usiku, kiongozi wa taifa alisema ni mapema sana kuanza kukadiria mafanikio ya serikali yake, akiwataka wakenya kumpa muda hadi mwaka 2027.
Akizungumza kuhusu uwanja wa Ruring’u ulio katika kaunti ya Nyeri, Rais Ruto alisema mradi huo ulikwamwishwa na kesi mahakamani kati ya mwanakandarasi na serikali, akidokeza kuwa kesi hiyo sasa imekamilika na ujenzi wake utaendelea.
Alisema amealika vikosi vya ulinzi nchini KDF, kutekeleza ujenzi wa uwanja huo na kwamba ujenzi wake utakamilika kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
“Nimeambia wanajeshi wakuje wasaidie kukamilisha ujenzi wa uwanja wa Ruring’u. Nina hakika ujenzi huo utakamilika kufikia mwishoni mwa mwaka huu,” alisema Rais Ruto.
Kuhusu ujenzi wa barabara ya MauMau inayounganisha kaunti za Kiambu, Murang’a na Nyeri, kiongozi wa taifa alisema ujenzi huo utakamilika kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao mwaka 2027.
“Si nilisema nitamaliza hizi barabara za Maumau, mtihani uko 2027, mniulize kuhusu barabara za Maumau wakati huo, kama kuna barabara nilianzisha haitakuwa imekamilishwa, si wananchi watajuwa vile watafanya. Lakini sasa mnachukua mtihani wa 2027, mnaleta sahii mwaka wa 2025,” alisema Rais Ruto.
Na kuhusu daraja la Nithi katika kaunti ya Tharaka Nithi ambapo mamia ya watu wamefariki kutokana na ajali za barabarani, Rais Ruto alisema wahandisi tayari wanakadiria ujenzi upya wa daraja hilo, na hivi karibuni daraja hilo litajengwa kuepusha ajali za barabarani.
“Hii Nithi Bridge tutaishughulikia…..wahandisi wamechora ramani mbili ya daraja hilo. Moja itagharimu shilingi bilioni tano na nyingine shilingi bilioni 50. Kwa hivyo tuko na mpango tayari wa jinsi tutashughulikia daraja hilo,” alidokeza kiongozi wa taifa.
Rais Ruto anaanza ziara ya siku tano katika eneo la Mlima Kenya leo Jumanne, akitarajiwa kuzindua na kukagua miradi ya maendeleo katika eneo hilo.