Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema atawania muhula wa nne katika uchaguzi wa rais mwaka ujao.
“Ndiyo, hakika mimi ni mgombea,”Bw Kagame aliambia jarida la lugha ya Kifaransa la Jeune Afrique Jumanne.
Alipoulizwa kuhusu nchi za Magharibi zitachukulia vipi uamuzi wake wa kugombea tena, Bw Kagame alisema, “Samahani kwa nchi za Magharibi, lakini kile ambacho nchi za Magharibi hufikiri si tatizo langu”.
“Nimefurahishwa na imani ambayo Wanyarwanda wanayo kwangu. Nitawatumikia daima, kadri niwezavyo.”
Bw Kagame alitania mwezi Aprili kwamba anatazamia kustaafu na kukabidhi madaraka baada ya miaka 23 madarakani.
Chama tawala nchini humo, Rwandan Patriotic Front (RPF-Inkotanyi), kilimuacha Bw Kagame kuendelea kuhudumu kama mwenyekiti wake mwezi Aprili.Ameongoza chama hicho tangu 1998.
Bw Kagame amekuwa rais wa taifa hilo la Afrika Mashariki tangu mwaka wa 2000. Kura ya maoni iliyozua utata mwaka 2015 iliondoa ukomo wa mihula miwili ya kikatiba kwa marais.
Alishinda uchaguzi uliopita wa 2017 kwa 98.8% ya kura.
Rwanda chini ya Rais Kagame imekuwa na utulivu wa kisiasa lakini wakosoaji na makundi ya haki za binadamu yanaituhumu serikali yake kwa kuweka mipaka ya uhuru wa kisiasa na kukandamiza upinzani.