Shirikisho la kandanda nchini Nigeria (NFF), limemteua Eric Chelle kuwa kocha mpya wa timu ya taifa almaarufu Super Eagles.
Chelle ambaye ni kocha wa zamani wa Mali amepewa jukumu la kuifuzisha Nigeria kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026.
Chelle anatwaa ukufunzi wa Super Eagles kutoka kwa Finidi George,aliyejiuzulu kufuatia matokeo mabaya katika mechi za kufuzu kwa kombe la Dunia mwaka 2026 ikiwemo sare dhidi ya Afrikka Kusini, na kushindwa na Benin.
Kocha huyo mpya ana kibarua kigumu akihitaji kusajili ushindi katika mechi mbili zilizosalia za kufuzu kwa Kombe la Dunia,mwezi Machi mwaka huu dhidi ya Rwanda ugenini na kuwaalika Zimbabwe.
Chelle, aliye na umri wa miaka 47 anajivunia tajriba pana ikiwemo kuiongoza Mali hadi robo fainali ya kombe la AFCON mwaka 2023, waliposhindwa na wenyeji Cote d’Ivoire.
Kwa Jumla chelle ameshinda mechi 14 kupiga sare 5 na kushindwa mechi tatu.