Nigeria itamenyana na Japani katika fainali ya Kombe la Dunia kwa wasichana walio chini ya umri wa miaka 17 katika kipute kinachoendelea nchini Morocco.
Flamingoes ya Nigeria walifuzu kwa fainali ya kombe hilo kwa mara ya kwanza kufuatia ushindi wa magoli 3-1 dhidi ya Brazil katika nusu fainali ya pili Jumatano jioni.
Awali, Japan wanaowinda kombe la pili na la kwanza tangu mwaka 2014, walijikatia tiketi ya fainali baada ya kuwatema nje mabingwa watetezi Korea Kaskazini mabao 4-1 kupitia matuta ya penalti baada ya sare ya goli moja katika muda wa kawaida.
Sawia na makala ya mwaka jana, Brazil watarejea kucheza mechi ya kuwania nishani ya shaba dhidi ya Korea Kaskazini.