Serikali imetoa makataa ya hadi Disemba 31 mwaka huu kwa wote wanaotengeneza dawa za binadamu kuafiki viwango vya kimataifa vya GS1.
Viwango hivyo vinalenga kuhakikisha usalama, uhalali na ufuatiliaji wa dawa na bidhaa zingine za afya.
Katibu wa Huduma za Matibabu Dkt. Ouma Oluga alitoa makataa hayo alipokutana na wadau wa utengenezaji na uuzaji dawa siku ya Jumatano jijini Nairobi.
Kikao hicho kiliwaleta pamoja Mafamasia, wadhibiti uuzaji na usambazaji dawa na mashirika ya kiserikali.
Dkt. Oluga, aliyemwakilisha Waziri wa Afya Aden Duale, alisema mfumo wa kitaifa wa usambazaji bidhaa na huduma wa (NLMIS) utawezesha bidhaa zozote za dawa kufuatiliwa kutoka kwa watengenezaji, Mafamasia hadi kwa watumiaji.
Hatua hiyo inadhamiriwa kumaliza changamoto ya ongezeko la dawa ghushi sokoni.