Mfanyabiashara maarufu mitandaoni nchini Tanzania Jenifer Jovin Bilikwija maarufu kama Niffer na mtangazaji wa redio Diva Gissele Malinzi wamekamatwa na maafisa wa polisi.
Kosa la wawili hao ni kuchangisha fedha za kusaidia waathiriwa wa mkasa wa kuporomoka kwa jengo katika eneo la Kariakoo, Dar es Salaam nchini Tanzania.
Ajali hiyo ilitokea Novemba 16, 2024.
Maafisa wa polisi jijini Dar es Salaam wametoa taarifa wakisema kwamba wawili hao walikuwa wanakusanya pesa kwa kutumia akaunti zao binafsi bila idhini yoyote.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam sasa litashirikiana na idara nyingine za kisheria nchini Tanzania ili kuhakikisha wawili hao wanachukuliwa hatua stahiki.
Polisi wanaendelea kutoa tahadhari kwa umma na kuonya kwamba watachukua hatua za kisheria kwa yeyote anayetumia majanga kujinufaisha.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila naye alikuwa ametoa onyo kali dhidi ya ukusanyaji wa pesa bila idhini alipozuru eneo la mkasa.
Kulingana na wakili Jebra Kambole aliyehojiwa na Clouds Fm, adhabu ya kosa hilo la kuchangisha fedha bila idhini ni kifungo cha mwaka mmoja gerezani.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyeongoza hafla ya kuaga miili ya waliofariki kwenye mkasa huo aliagiza kukamatwa kwa wahusika wa michango hiyo.
Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa ametangaza awali kwamba serikali itagharamia mazishi na matibabu ya walioathirika na mkasa huo.