Nicole Berry afikishwa mahakamani

Mwigizaji huyo alikamatwa Jumatatu wiki iliyopita kwa kuchangisha pesa bila kibali.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwigizaji wa Tanzania Joyce Mbaga ambaye wengi wanamfahamu kama Nicole Berry leo alifikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi ya Kinondoni Jijini Dar es salaam nchini Tanzania.

Alisomewa mashtaka dhidi yake ya kuendesha genge la uhalifu na kupokea pesa shilingi milioni 185.5 za Tanzania kutoka kwa umma bila kibali kutoka Benki Kuu ya Tanzania.

Mshtakiwa wa pili kwenye kesi hiyo ni Rehema Mahanhu na wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Julai 2024 na Machi 2025 ndani ya Mkoa wa Dar es salaam.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 24,2025 na washtakiwa kurejeshwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili na pesa taslimu shilingi milioni 46.3 au hati ya mali isiyohamishika ya thamani hiyo.

Nicole na mwenzake wanatuhumiwa kwa kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu kwa kubuni makundi kwenye Whatsapp na kuchangisha fedha kutoka kwa umma bila kibali, na baadaye kutokomea na pesa hizo.

Mbaga alikamatwa Machi 3, 2025 na kulingana na maafisa wa polisi jijini Dar es Salaam, watu zaidi ya 16 walilalamikia kulaghaiwa naye.

Hii sio mara ya kwanza mtu maarufu anakamatwa nchini Tanzania kwa kuchangisha pesa bila kibali. Mwezi Novemba mwaka jana, mfanyabiashara Niffer alikamatwa kwa sababu hiyo.

Hii ni baada yake kubuni kundi la Whatsapp na kuanza kuchangisha pesa za kusaidia watu ambao walikuwa wamehusika kwenye mkasa wa jengo kuporomoka huko Kariakoo.

Lakini aliachiliwa baada ya kuomba masamaha.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *