Waziri wa Michezo Kipchumba Murkomen ameweka bayana kuwa wizara yake haitaruhusu viongozi wa sasa wa FKF wakiongozwa na Rais Nick Mwendwa kuwania muhula wa tatu kwenye uchaguzi ulioratibiwa kufanywa mwezi Disemba mwaka huu.
Murkomen amesema maafisa wa sasa wa FKF ambao wamehudumu kwa kipindi cha miaka minane afisini ni sharti wazingatie sheria za michezo za mwaka 2013.
Sheria hizo haziruhusu mtu kuwa afisini kwa zaidi ya mihula miwili ya miaka minne kila moja katika wadhifa mmoja.
Akijibu maswali bungeni siku Jumatano, Waziri amesimama kidete kuwa walio afisini kwa sasa watawania nyadha tofauti.
Hatua hii ina maana kuwa Mwendwa pamoja na kamati kuu watapoteza viti vyao.
Haya yanajiri siku mbili tu baada ya kutangazwa kwa bodi mpya ya uchaguzi huku uchaguzi huo ukitarajiwa kuandaliwa kufikia katikati ya mwezi Disemba mwaka huu.