Rais William Ruto ameutaka upinzani kukoma kuitumia vibaya demokrasia ya nchi kupitia maandamano yenye vurugu.
Amesema kifungu cha katiba kinachoruhusu maandamano sharti kitekelezwe kwa amani bila kusababisha madhara kwa maisha na mali ya watu.
“Hatuna tatizo lolote kabisa kuhusu kifungu chochote kinachohusu maandamano lakini hatuwezi tukageuka kuwa nchi ya machafuko, hatuwezi tukawa nchi ya vurugu na hakuna yeyote anayepaswa kutumia kifungu cha katiba kusababisha vurugu na kuharibu mali ya umma na kusababisha vifo,” alisema Rais Ruto wakati akizungumza mjini Kericho jana Jumatano.
Alisema suluhisho ya gharama ya juu ya maisha imejikita kwenye mpango wa kimakati wa kiuchumi wa serikali ya Kenya Kwanza wala si maandamano.
“Ni lazima tuilinde nchi yetu na demokrasia yetu kwa kuhakikisha siasa zetu hazina machafuko na uharibifu wa mali. Ni lazima tuilinde nchi hii na polisi lazima wawakalie ngumu wahalifu na majangili wanaotaka kuharibu biashara ya watu wengine. Polisi wana wajibu wa kulinda mali ya kila Mkenya na maisha.”
Ruto aliutaka upinzani kuwaslisha malalamishi yao kupitia njia zinazofaa badala ya kushiriki maandamano yenye vurugu, akiongeza kuwa majadiliano yoyote yanapaswa kuhusu masuala yanayowaathiri Wakenya.
“Tuko tayari kufanya mazungumzo alimuradi yanahusu masuala ya Wakenya wala si ugavi wa mamlaka.”