Bunge la taifa limetangaza kuwa litakata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu, ulioharamisha hazina ya ustawi wa maeneo bunge NGCDF.
Kupitia kwa taarifa, bunge hilo lilisema limewaagiza mawakili wake, kupinga uamuzi huo wa mahakama uliotolewa Ijumaa, na jopo la majaji watatu ambao ni; Kanyi Kimondo, Roselyn Aburili, na Mugure Thande.
“Katika rufaa hiyo, bunge la taifa linalenga kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusiana na uhalali wa kikatiba wa sheria ya hazina ya NGCDF ya mwaka 2015,” ilisema taarifa hiyo ya bunge.
Uamuzi huo wa mahakama ulidokeza kuwa hazina ya NG-CDF, ilikiuka maadili ya fedha za umma na mgawanyo wa madaraka.
Majaji hao waliongeza kuwa hazina hiyo inahitilafiana na majukumu yaliyogatuliwa, na kusababisha kurejelewa kwa kushughuli na utumizi mbaya wa rasilimali.
Hata hivyo mahakama hiyo ilisema hazina hiyo itaendelea kufanya kazi hadi Juni 26,2025 ili kutoa fursa ya kukamilishwa kwa miradi inayoendelea ambayo inafadhiliwa na hazina hiyo.