Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anataka raia wa Eritrea ambao walihusika kwenye maandamano yaliyoghubikwa na vurugu jijini Tel Aviv warejeshwe nchini kwao mara moja na ameamuru pia mpango wa kuondoa wahamiaji wote wa mataifa ya Afrika kutoka kwa nchi hiyo.
Matamshi ya Netanyahu yanafuatia vurugu mbaya za makundi hasimu ya raia wa Eritrea katika eneo kusini la mji wa Tel Aviv ambapo watu wengi walipata majeraha.
Raia wa Eritrea wanaitafuta hifadhi nchini Israel wanaounga mkono serikali ya nchi yao na wanaoipinga walizozana na kupigana jijini Tel Aviv wakitumia mbao, vyuma na mawe.
Waliharibu mali wakati wa vurugu hizo kama vile magari na madirisha ya maduka jambo ambalo lililazimu polisi wa kupambana na ghasia kuwarushia vitoza machozi, guruneti na hata risasi kwa nia ya kutuliza hali.
Vurugu hizo za raia wa Eritrea zimefufua suala sugu la wakimbizi ambalo limesababisha mgawanyiko nchini Israel. Zimejiri wakati Israel imegawanyika kuhusu mpango wa Netanyahu wa kufanya mabadiliko katika idara ya mahakama na wanaomuunga mkono wanahisi kwamba wakimbizi ndio sababu kubwa ya kutaka kubadilisha idara hiyo kwani inaaminika kuwa kikwazo katika kuondoa wakimbizi nchini humo.
Kulingana na sheria ya kimataifa serikali ya Israel haiwezi kuwafukuza wakimbizi warejee kwenye nchi ambapo maisha yao au uhuru umetishiwa.
Wakimbizi wapatao elfu 25 kutoka nchi za Afrika wanaishi nchini Israel, wengi wakiwa raia wa nchi za Sudan na Eritrea waliotoroka mapigano.