Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kwamba yuko tayari kwa mpango wa kusitisha vita kwa kiwang fulani na wala sio kabisa ili kuruhusu kuachiliwa kwa mateka ambao wameshikiliwa huko Gaza hata kama sio wote.
Alisisitiza kwamba hatakubali mpango wowote wa kusitisha vita kabisa hata baada ya Marekani kusema awali kwamba, mpango wa kusitisha vita utakaopendekezwa na Israel utakuwa njia ya kumaliza vita kabisa.
Katika mahojiano kwenye runinga jana Jumapili, Netanyahu alisema kwamba lengo kuu ni kuafikia uhuru wa mateka na kung’oa kabisa utawala wa Hamas katika ukanda wa Gaza.
Huku haya yakijiri, maelfu ya raia wa Israel wamekuwa wakifanya maandamano kulalamikia maamuzi ya Netanyahu na serikali yake kuhusu vita vya Gaza wakitaka uchaguzi uandaliwe mapema na mateka waachiliwe huru.
Rais wa Marekani Joe Biden alitangaza pendekezo la kusitisha vita vya Gaza mwezi uliopita, ambapo mapigano yangesitishwa kwa majuma 6 na mateka wa pande zote mbili kuachiliwa huru.
Biden anaamini kwamba ubadilishanaji wa mateka utatoa fursa ya mazungumzo ya kusitisha vita kabisa.
Netanyahu alisema pia kwenye mahojiano kwamba mashambulizi makali ya wanajeshi wa Israel katika mji wa Rafah ambao uko katika eneo la kusini la ukanda wa Gaza yanakaribia mwisho.
Mapigano yameshuhudiwa katika ukanda wa Gaza kwa miezi minane sasa na yalianza kama njia ya Israel kulipiza kisasi baada ya kushambuliwa na wanachama wa kundi la Hamas Oktoba 2023.
Watu zaidi ya elfu 37 wameuawa huko Gaza kufikia sasa.