Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekataa mpango wa mapatano ya kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza uliopendekezwa na kundi la Hamas.
Kundi la Hamas lilipendekeza kwamba pande zote zisitishe vita, ziachilie wafungwa wa vita hivyo, wanajeshi wa Israel waondolewe Gaza na Israel itambue kundi la Hamas kama linalotawala Ukanda wa Gaza.
Netanyahu anayekabiliwa na shinikizo za kurejesha mateka wa Israel kutoka Gaza wanaoshikiliwa na wapiganaji wa Hamas amekataa mpango huo akisema ni kama kukubali kushindwa.
Anasema pia kwamba kukubali mpango huo ni kuacha kundi la Hamas likiwa imara na kwamba wanajeshi wa Israel walikufa bure.
Kulingana naye, mpango huo ukikubaliwa, usalama wa raia wa Israel utatishiwa na hawataweza pia kurejesha mateka nyumbani.
Jana Jumapili jioni, jamaa wa mateka wa Israel na wa wasiojulikana waliko waliandamana nje ya makazi ya kibinafsi ya Netanyahu mjini Jerusalem, wakiapa kutoondoka hadi mapatano ya kuachiliwa kwa mateka hao yaafikiwe.
Mwezi Novemba mwaka jana, kundi la Hamas liliachilia huru mateka 100 huku Israel ikiachilia mateka wa Palestina chini ya mpango wa muda mfupi wa kusitisha mapigano.
Mpango huo uliafikiwa kupitia majadiliano yaliyoongozwa na Misri, Qatar na Marekani.
Israel inaamini kwamba raia wake 136 bado wanazuiliwa na Hamas hadi sasa.
Wapalestina wapatao elfu 25,105 wanaaminika kufa kwenye mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza baada ya wapiganaji wa Hamas kushambulia Israel Oktoba 7, 2023.