Mmiliki wa mtandao wa kijamii wa Twitter Elon Musk amesema atabadili nembo ya mtandao huo. Aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao huo huo kwamba hivi karibuni tutapigia kwaheri nembo ya mtandao huo ambayo ni ndege.
Musk alibadilisha jina la kampuni inayomiliki Twitter na kuiita “X Corp” na alichapisha video fupi inayoonyesha nembo ya herufi “X”.
Aliendelea kusema kwamba iwapo wangechapisha nembo nzuri kabisa ya heruf hiyo basi ingeanza kutumika kote ulimwengini mara moja.
Elon alithibitisha mipango ya kubadilisha nembo ya Twitter kwenye mkutano mmoja uliokuwa ukifanyika kwenye jukwaa la mtandao huo almaarufu “Twitter Spaces” ambapo alijibu “ndio” alipoulizwa iwapo nembo ya Twitter itabadilika.
Mwezi Aprili mwaka huu, nembo ya Twitter ilibadilika kwa muda mfupi na kuwa ya mbwa.
Twitter imekuwa ikisuasua tangu Musk alipoinunua mwezi Oktoba mwaka jana na amekuwa akikashifiwa na watumizi na wataalamu kwa mabadiliko ambayo amekuwa akitekeleza.
Alianzisha mchakato wa watumizi kulipia uthibitisho wa kurasa zao na baadaye akaweka kiwango cha jumbe ambazo kila mtumizi anaweza kufikia na kusoma kwa siku.
Misukosuko ya Twitter ilisababisha kukua kwa mtandao pinzani unaomilikiwa na kampuni ya Meta uitwao “Threads” ambao ulijipatia watumizi milioni 100 katika siku tano za kwanza baada ya kuzinduliwa.
Matatizo ya Twitter yanazidi kuongezeka la hivi punde zaidi likiwa kesi dhidi yake kuhusu kutolipa waliokuwa wafanyikazi wake, malipo ya kuwastaafisha.