Ndugu na dada wamehukumiwa vifungo vya muda mrefu gerezani na hakimu wa mahakama ya wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu nchini Tanzania kutokana na kosa la kushiriki tendo la ndoa.
Katika kesi hiyo ya kusangaza, jamaa kwa jina Musa Shija wa miaka 32 na dadake aitwaye Hollo Shija wa miaka 36 walihukumiwa miaka 20 na 30 jela mtawalia.
Wawili hao ambao ni watoto wa mama mmoja na baba mmoja yaani ndugu wa damu walitenda kosa hilo kiasi cha kupata mtoto.
Hakimu mkazi wa mahakama hiyo ya Maswa alielezea kwamba mahakama iliridhika vya kutosha baada ya kusikiliza ushahidi, kwamba wawili hao ambao ni wakulima na wakazi wa kijiji cha Mandang’ombe walitekeleza kosa hilo.
Makosa hayo yalithibitishwa kupitia vielelezo kadhaa vilivyojumuisha vipimo vya msimbojeni, yaani DNA na ushuhuda wa mashahidi 11.
Hakimu alielezea kwamba hatua ya ndugu kujamiiana ni kinyume na kifungu nambari 158 sehemu kwanza (b) na kifungu nambari 160 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 6, marejebisho ya mwaka 2022.
Kwa mujibu wa maelezo ya upande wa mashtaka washtakiwa waliishi pamoja kama Mume na Mke na wakapata Mtoto mmoja, mwaka 2018 hadi Julai 2024.
Walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Agosti 12,2025 na kukiri makosa yao.
Hukumu dhidi ya wawili hao ilitolewa wakati huo lakini wakakata rufaa katika mahakama kuu ambayo iliamuru kesi isikilizwe upya.
Kesi hiyo ilianza tena Mei 06,2025 ambapo walikanusha makosa dhidi yao hata baada ya ushahidi kama wa vinasaba.
Wanashikiliwa kwamba wao ni wanandoa halali na kwamba Mzee Shija Kamuga sio baba yao halisi bali ni jirani mwenye chuki. Mussa anasema alimwoa Horro kihalali na kumtolea mahari ya elfu 325 pesa za Tanzania.