Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro amepuuzilia mbali uwezekano wa kuwa na serikali ya muungano licha ya mazungumzo yanayoendelea kati ya timu za Kenya Kwanza na Azimio.
Mazungumzo hayo yanaongozwa na mbunge wa walio wengi katika bunge la taifa Kimani Ichung’wah na kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka.
Hata hivyo, Nyoro anasema serikali haitashinikizwa na upinzani kuunda serikali ya muungano.
Badala yake, anatoa wito kwa Wakenya kuunga mkono utawala wa Rais William Ruto kwani una mpango madhubuti wa kuwafaidi.
Kulingana naye, kuna mafanikio mengi ambayo serikali ya Kenya Kwanza imeafikia kwa kipindi cha mwaka mmoja ambao imekuwa madarakani, hususan katika nyanja za elimu, afya, uchumi na usalama.
Mbunge huyo wa Kiharu aidha amewataka Wakenya kutowasikiliza watu ambao kazi yao ni kuiharibia serikali sifa kwa lengo la kupunguza kasi ya maendeleo.
Kauli zake ziliungwa mkono na mwakilishi wa wanawake katika bunge la taifa Jane Kagiri aliyesifia kurejeshwa kwa amani katika maeneo yanayokumbwa na wizi wa mifugo na kuajiriwa kwa polisi wa akiba.
Nyoro na Kagiri walisema hayo leo Alhamisi katika eneo bunge la Laikipia Mashariki, kaunti ya Laikipia.
Matamshi yao yanawadia siku moja baada ya kura ya maoni iliyofanywa na kampuni ya Infotrak kuonyesha kuwa asilimia 55 ya Wakenya wanaunga mkono utendakazi wa Rais Ruto.
Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 65 ya Wakenya wanaitaka serikali ya Kenya Kwanza kulipa kipaumbele suala la kupanda kwa gharama ya maisha.
Serikali tayari inasema inashughulikia suala hilo kupitia utoaji wa bei ya mbolea nafuu kwa wakulima.
Mbolea hiyo kwa sasa inauzwa kwa shilingi 2,500 kwa gunia moja, ikishuka kutoka bei ya shilingi 7,000 ya wakati wa utawala uliopita.
Kutokana na kutolewa kwa mbolea hiyo, Rais Ruto anasema nchi hii inatarajiwa kuvuna mahindi magunia milioni 61 mwaka huu.
Hili litakuwa ongezeko la magunia milioni 17 ikilinganishwa na magunia milioni 44 yaliyovunwa mwaka jana.
“Mwaka uuliopita, tulivuna magunia milioni 44 kwa sababu wakulima hawakuweza kugharimia bei ya mbolea ambayo ilikuwa juu sana. Lakini mwaka huu, kwa sababu tumeweka mpango mzuri, tumepunguza gharama ya mbolea, mavuno ambayo tunatarajia ambayo yameanza kuja ni magunia milioni 61,” Rais Ruto alinukuliwa akisema awali.