Ndege moja ndogo ilianguka katika mji unaopendwa sana na watalii nchini Brazil na kuua watu wote 10 waliokuwemo huku wengine zaidi ya 12 wakiachwa na majeraha.
Ndege hiyo iliangukia dohani au bomba la moshi la nyumba moja na orofa ya pili ya nyumba nyingine kabla ya kuishia kwenye duka katika eneo la Gramado muda mfupi baada ya kupaa kutoka Canela.
Gavana wa eneo la Rio Grande do Sul Eduardo Leite aliambia wanahabari kwamba mmiliki wa ndege hiyo ambaye pia alkuwa akiiendesha Luiz Claudio Galeazzi, alifariki pamoja na watu wengine tisa wa familia yake.
Leite aliongeza kwamba watu 17 ambao walikuwa wanaendelea na shughuli zao waliumia kwenye ajali hiyo huku 12 kati yao wakisalia hospitalini kwa matibabu.
Kampuni ya mmiliki huyo wa ndege iitwayo Galeazzi & Associados, ilithibitisha kwamba mkubwa wao, mke wake na binti zao watatu walifariki kwenye ajali hiyo ya ndege.
Mji wa Gramado, ulio kwenye milima ya Serra Gauchani maarufu sana kwa watu wanaotaka eneo la kutulia kwa likizo hasa msimu wa Krismasi.
Ajali hii inajiri zaidi ya mwaka mmoja tangu Brazil ilipokumbwa na ajali mbaya zaidi ya angani wakati ndege yenye injini mbili ilianguka katika mji wa Vinhedo, na kuua watu wote 62 waliokuwemo.