Tume ya kitaifa ya utangamano na mshikamano NCIC imelaani vikali semi za chuki zilizotolewa na Khalef Khalifa, mkurugenzi wa shirika la waisilamu kuhusu haki MUHURI.
NCIC imetaja matamshi hayo kuwa ya kuzua migawanyiko na hatari.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, mwenyekiti wa NCIC Samuel Kobia, alisisitiza kwamba maneno ya Khalifa yaliyonakiliwa kwenye video yanatishia amani na umoja, vitu ambavyo wakenya wameng’ang’ana kuafikia kwatika muda wa miaka mingi.
Kulingana na Kobia semi kama hizo ambazo zinaweza kuchukuliwa kuwa uchochezi wa vurugu na chuki ya kikabila hazina nafasi katika taifa la Kenya.
Aliongeza kusema kwamba maneno kama hayo yanakinzana na kifungu nambari 33 cha katiba ambacho kinaangazia uhuru wa kujieleza.
Kobia alisisitiza kwamba kila mkenya ana haki ya kuishi, kufanya kazi na kujihusisha na shughuli za umma bila woga wa kubaguliwa kwa misingi ya kabila, dini au mwegemeo wa kisiasa.
Tume ya NCIC imeanzisha uchunguzi kuhusu usemi wa Khalifa huku akitakiwa kufika mbele ya tume hiyo Disemba 9, 2024 kufafanua kuhusu semi hizo.
Mwenyekiti huyo ametangaza pia mipango ya kuandaa kikao cha amani huko Lamu kitakachohusisha viongozi wa siasa, viongzi wa dini na wawakilishi wa wakazi kuhimiza amani na kuondoa vitisho.