Baraza la Kitaifa la Makanisa Nchini, NCCK limetoa wito kwa serikali ya Kenya Kwanza kusikiliza vilio vya waandamanaji wanaopinga Mswada wa Fedha 2024.
Waandamanaji hao hasa vijana wiki iliyopita walijitokeza kwa wingi katika miji mbalimbali kupinga mswada huo wanaosema utafanya hali ya maisha kutostahimilika.
Wamepanga msururu wa maandamano mengine wiki hii kupinga mswada huo huku wengi wakitarajiwa kujitokeza kwa wingi kesho Jumanne, siku ambayo wabunge wanatarajiwa kupiga kura ya ama kuupitisha au kuukatalia mbali mswada huo.
NCCK pia inataka polisi kuepuka kuwafanyia ukatili waandamanaji wasiokuwa na silaha wakati wa maandamano hayo.
Katika taarifa iliyosomwa katika makanisa wanachama wa NCCK kote nchini, viongozi wa kidini wa makanisa hayo walitoa wito kwa wabunge kusikiliza malalamishi ya Wakenya na kujizuia kuupitisha mswada huo jinsi ulivyo kwa sasa.
Mchungaji David Muthuiya ambaye pia ni Katibu wa NCCK katika kaunti ya Isiolo aliutaja Mswada wa Fedha 2024 kuwa kandamizi na unaokusudia kuwawekea Wakenya ambao tayari wameelemewa na gharama ya juu ya maisha mzigo mkubwa wa ulipaji ushuru.
Mchungaji Muthuiya alisema serikali na taasisi zingine za jamii zipo kuwapatia watu matumaini na kuwasaidia kujiendeleza kama watu binafsi na jamii na kwamba kuwatoza ushuru kupindukia kunaenda kinyume cha matarajio hayo.
Aliongeza kuwa ingawa ni wajibu wa raia kuunga mkono shughuli za serikali kupitia ulipaji kodi, serikali kwa upande mwingine haipaswi kuwakandamiza kwa kuwatoza ushuru kupindukia, akitaja ushuru uliopendekezwa wa mkate na magari.
Mchungaji Muthuiya alisema maandamano ya vijana wanaofahamika sana kama Gen Z yanaakisi hisia za Wakenya wengi kuhusiana na mswada huo.