Mwanamuziki wa Kenya Nazizi amemkumbuka mwanawe aliyeaga dunia kwa jina Jazeel Adam. Msanii huyo alichapisha picha ya mtoto huyo kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii.
“Hujambo kisura maisha yamebadilika sana tangu uliponiacha. Hakuna kilicho na maana hata neno Familia limebadilika katika fikra zangu” aliandika.
Aliendelea kwa kumpa Jazeel ripoti ya maisha yake akisema ndugu yake aitwaye Tafari Firoz alikwenda shule ya soka na sasa nyumba huwa kimya na yenye upweke.
“Mama huwa hana furaha siku nyingi na huwa anatumia muda wake mwingi akilia akitamani mambo yangekuwa tofauti. Natamani ningerudia siku ile lakini siwezi na nililobaki nalo ni kumbukumbu na picha” aliendelea kusema katika ujumbe huo.
Jazeel aliaga dunia mwezi Disemba mwaka 2023 wakati Nazizi na familia yake walikuwa likizo nchini Tanzania, tukio ambalo lilimvunja moyo sana mwanamuziki huyo.
Disemba mwaka jana wakati wa kupiga picha kama fanilia, Nazizi alimkumbuka tena mtoto huyo akisema, “Kupigwa picha bila wewe kunaumiza moyo sana, sisi wote tulidodonkwa na machozi wakati wa kupigwa picha hizi.”
Alisema angekuwepo angeongeza vicheko huku kila mmoja akijaribu kumdhibiti kama ilivyokuwa awali katika shughuli nyingine za kupiga picha za familia.