Nathaniel Bassey kuimba katika kikao cha kabla ya uapisho wa Rais Trump

Bassey alichapisha bango la kikao hicho cha kiamsha kinywa kwenye akaunti yake ya Instagram na kuandika, "Tuinue sauti nchini Marekani. Na Mfalme wa Utukufu aingie. Tuonane Januari 20, 2025."

Marion Bosire
2 Min Read

Mwimbaji wa nyimbo za injili kutoka Nigeria Nathaniel Bassey amealikwa kuimba katika kikao cha kiamsha kinywa cha rais mteule wa Marekani Donald Trump, Januari 20, 2025.

Kulingana na taarifa, mhubiri Merrie Turner ataandaa kikao hicho kisicho cha serkali na kisicho cha kisiasa kabla ya Trump na J.D Vance kuapishwa rasmi kama Rais na Naibu Rais wa Marekani.

Lengo kuu la kikao hicho kulingana na waandalizi, ni kutoa usaidizi wa kiroho kwa serikali ijayo kupitia maombi na ibada.

Mwimbaji huyo ambaye pia ni mhubiri mzaliwa wa jimbo la Akwa Ibom amewahi kuhudumu nchini Marekani ambapo mwaka uliopita wa 2024, Meya wa Albany, huko New York, aliipa tarehe 6 Oktoba jina lake.

Nathaniel Bassey, amepata kufahamika ulimwenguni kote kwa nyimbo zake kama vile ‘Imela’, ‘Onise Iyanu’, na ‘Olowogbogboro’.

Bassey alichapisha bango la kikao hicho cha kiamsha kinywa kwenye akaunti yake ya Instagram na kuandika, “Tuinue sauti nchini Marekani. Na Mfalme wa Utukufu aingie. Tuonane Januari 20, 2025.”

Kulingana na bango hilo kikao hicho kitaanza saa moja asubuhi na kukamilika saa saba mchana, saa za Marekani, katika hoteli ya Waldorf Astoria, barabara ya 1100 Pennsylvania, jijini Washington DC.

Siku hiyo hiyo ndiyo Trump na Vance watakula kiapo rasmi kabla ya kuanza kuhudumu kama viongozi wa Marekani, hafla rasmi ikitarajiwa kuanza saa tatu asubuhi huko Capitol, jijini Washington DC.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *