Mwanamitindo Naomi Campbell amepigwa marufuku kuwa mdhamini wa shirika moja la kutoa misaada, baada ya kugunduliwa kuwa fedha za shirika hilo zilitumika katika hoteli za kifahari na kwa huduma za ususi.
Uchunguzi wa Tume ya shirika hilo uligundua kuwa shughuli za maonyesho ya mitindo kwa ajili ya usaidizi hazikufanyika kwa kiasi kikubwa cha pesa kilichopatikana kama ilivyotakiwa.
Badala yake zilitumika kwa ununuzi wa sigara na usalama wa Campbell na malipo mengine ambayo hayajaidhinishwa kwa mmoja wa wadhamini wenzake wa shirika hilo.
“Nimegundua leo kuhusu ugunduzi huo, na nina wasiwasi mkubwa,” Campbell, 54, aliliambia shirika la habari la AP.
Aliongeza kuwa yeye sio mtu “aliyekuwa na udhibiti” wa shirika hilo la kutoa misaada.
Amepigwa marufuku kujihusisha na shirika hilo kwa miaka mitano huku wadhamini wengine wawili, Bianka Hellmich na Veronica Chou, wakipigwa marufuku kwa miaka tisa na minne mtawalia.