Namwamba ampeleka Dahir Kisumu kwa ndege kushiriki kipute cha CECAFA U-18

Tom Mathinji
2 Min Read

Dahir Abdikadir ana kila sababu ya kutabasamu baada ya kupata fursa adimu ya kusafiri kwa ndege hadi kaunti ya Kisumu na Waziri wa Michezo Ababu Namwamba. 

Mchezaji huyo anayechipukia atashiriki mashindano ya CECAFA U-18 yatakayoshirikisha wachezaji wenye umri chini ya miaka 18.

Mashindano hayo yataandaliwa katika kuanti za Kisumu na Kakamega kuanzia kesho Jumamosi, Novemba 25 – hadi Disemba 8, 2023.

Dahir, mwenye umri wa miaka 17 ni mlinda lango wa timu ya Bula Pesa katika kaunti ya Mandera.

Ni mmoja wa wachezaji walionyesha talanta ya hali ya juu katika mashindano ya kanda  yaliyoandaliwa katika kaunti ya Nyeri.

Mwanafunzi huyo wa kidato cha pili katika shule ya upili ya wavulana ya St. Antony, Kitale alinufaika pakubwa baada ya kutambuliwa na kundi lililotumwa na Wizara ya Michezo lililojumuisha wachezaji tajika wa zamani akiwemo Alan Wanga, Musa Otieno, Winna Shilavula na Denis Onyango miongoni mwa wengine.

Wenyeji Kenya wameorodheshwa katika kundi A pamoja na Rwanda, Somalia na Sudan.

Kundi B linajumuisha  Sudan Kusini, Tanzania, Uganda na Zanzibar na michuano ya kundi hili itaandaliwa katika kaunti jirani ya Kakamega.

Mechi zote zitapeperushwa mbashara na runinga ya KBC Channel 1 na Y54 na kutangazwa kupitia Radio Taifa, Ingo FM na Mayienga FM.

Website |  + posts
Share This Article