Chipukizi walidhihirisha umahiri wao katika siku ya pili ya mkondo wa sita na wa mwisho wa mbio za uwanjani za chama cha riadha Kenya zilizokamilika leo katika uwanja wa michezo wa Ulinzi.
Bingwa wa kilomita sita katika mashindano ya mbio za nyika za Sirikwa Classic, Cynthia Chepkurui wa kambi ya Lemotit, alisajili muda wa kasi katika fainali za mita 5,000 wanawake akitumia dakika 15 sekunde 44.81, mbele ya mshindi wa nishani ya shaba ya dunia mwaka 2013, Mercy Cherono, aliyemaliza wa pili kwa muda wa dakika 15 sekunde 0, sekunde 7.46, mbele ya Diana Wanza aliyemaliza wa tatu.
Vivian Chebet wa KDF aliyeshiriki michezo ya Olimpiki alitumia dakika 2 sekunde 46.7 kuibuka mshindi wa mita 800,sekunde 0.01, mbele ya Naomi Korir wa Central Rift aliyemaliza wa pili huku Josephine Mancha wa kambi ya Magnolia, akihitimisha nafasi tatu bora kwa dakika 2:07.58 .
Mshindi wa nishani ya fedha ya dunia katika mashindano ya ukumbini Noah Kibet wa North Rift alitwaa ubingwa wa mita 800 kwa dakika 1 sekunde 45.98, akifuatwa na Cornelius Tuwei, kutoka KDF na Vincent Kibet wa Magereza kwa muda wa dakika 1:46.14 na 1:47.42 kwenye nafasi za pili na tatu mtawalia.
Wanariadha kutoka eneo la South Rift walitwaa nafasi zote tatu bora katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji wakiongozwa na Emmanuel Lemiso Someki, aliyetumia dakika 8 sekunde 45.20 kufika utepeni.
Peter Rono alimaliza wa pili kwa dakika 8:53.65 katika nafasi ya pili huku Cosmas Mutai, akiridhia nafasi ya tatu kwa muda wa dakika 8:55.63.
Mkondo wa leo unapisha mashindano ya uwanjani viwango vya kaunti Juni 7 na yale ya mikoa wiki moja baadaye.
Msimu wa mbio za uwanjani utakamilika kwa mashindano ya kitaifa baina ya Juni 27 na 28, ambayo pia yatatumika kuteua kikosi cha Kenya kitakachoshiriki mashindano ya riadha duniani katika mita 10,000.