Wizara ya Fedha imepata pigo baada ya kuamuliwa kwamba serikali ya kitaifa na zile za kaunti zigawane nakisi ya mgao wa bajeti.
Hii ni baada ya Kamati ya Upatanishi ya bunge la Seneti na lile la kitaifa kukataa pendekezo la kutaka nakisi hiyo ya pesa za matumizi kuachiwa serikali za ugatuzi.
Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro aliyeongoza kamati hiyo, alisema mzigo wa nakisi ya Pato la Taifa kamwe haupaswi kuachiwa serikali za kaunti.
Haya yanafuatia hatua ya Wizara ya Fedha kuagiza bunge kukata shilingi bilioni 20 kutoka kwa bajeti ya shilingi bilioni 400 zilizotengewa serikali za kaunti kufuatia kufutiliwa mbali kwa Mswada wa Fedha wa mwaka 2024.