Naibu Rais Rigathi Gachagua ahimiza umoja Mlima Kenya

Marion Bosire
1 Min Read

Naibu Rais Rigathi Gachagua amehimiza wakazi wa eneo la mlima Kenya wawe na umoja na upendo kila wakati akiongeza kusema kwamba kamwe hawezi kukubali yeyote kushambulia ndugu zake na dada zake.

Akizungumza kwenye hafla ya mazishi ya aliyekuwa mwalimu wake kwa jina Kano, huko Gichugu kaunti ya Kirinyaga, Gachagua alisema kwamba tangu jadi wasaliti na marafiki wa maadui hawakosi katika eneo la Mlima Kenya lakini anafurahia kwamba wengi wa wakazi huwa katika upande wa wazuri.

Alimsifia marehemu Mwalimu Kano akisema kwamba alikuwa shupavu na alimwelekeza maishani ndiposa akawa kiongozi.

“Marehemu Kano alinifundisha jinsi ya kujadili vyema wakati huo akisema ushupavu katika mijadala utanisaidia maishani. Ukweli ni kwamba ujuzi huo ulinisaidia sana wakati wa mjadala wa wawaniaji wa wadhifa wa naibu rais na dada Martha Karua.” alisema Gachagua.

Kiongozi huyo alihimiza kila mmoja kuheshimu walimu na kuwapenda akisema kwamba kila mmoja amefika aliko sasa maishani kutokana na adhabu na maelekezo aliyopata kutoka kwa walimu.

Gachagua alisema alifahamishwa kuhusu kifo cha Kano wakati alikuwa amechukua mapumziko ya siku saba kwa ajili ya kufunga na kuomba. Alisema alikuwa ameelekeza wasaidizi wake kwamba wasikubalie yeyote kuingilia mfungo wake lakini hawakuwa na jingine ila kumfahamisha.

Share This Article