Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki amewasili mjini Maputo nchini Msumbiji.
Prof. Kindiki amewasili nchini humo kuiwakilisha Kenya katika hafla ya uapisho wa Rais mteule wa nchi hiyo Daniel Chapo.
Rais mteule Chapo ataapishwa leo Jumatano katika hafla ambayo inatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka barani Afrika.
Mapema mwezi huu, Baraza la Kikatiba nchini Msumbiji lilitangaza kuwa Rais mteule Chapo ataapishwa Januari 15.
Hii ni baada ya Chapo kutangazwa mshindi wa uchaguzi uliofanywa mwezi Oktoba mwaka jana na ulioghubikwa na wingu zito la utata.
Upinzani umekuwa ukifanya maandamano tangu kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo ambayo unayapinga.
Imeiripotiwa kuwa takriban watu 290 wamefariki nchini humo kutokana machafuko ya baada ya uchaguzi.
Chapo wa chama tawala cha Frelimo alitangazwa mshindi kwa kupata asilimia 65.17 dhidi ya asilimia 24 za mpinzani wake wa karibu Venancio Mandlane.
Viongozi wa mataifa ya kusini mwa Afrika wamekuwa wakitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano huku wakihimiza mazungumzo ili kumaliza mzozo wa kisiasa kutoka kwa pande husika.