Naibu Rais Kithure Kindiki amepongeza washindi wa awamu ya 97 ya mashindano ya kitaifa ya muziki na utamaduni, iliyofanyika katika ukumbi wa Bomas.
Mashindano hayo yamefanyika kwa wiki nzima na yalishuhudia maonyesho ya sanaa ya Kenya na utamaduni kupitia nyimbo, densi, mashairi, maigizo na saa nyingine ibuka.
Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Mkuu wa Wafanyakazi katika Idara ya Utendakazi na Usimamizi katika Ofisi ya Rais Eliud Owalo, Kindiki alipongeza tamasha hilo kwa jukumu lake la kuimarisha ubunifu na talanta humu nchini.
“Kwa miaka 97 tamasha hili limetekeleza jukumu muhimu katika kuhifadhi na kusherehekea sanaa zetu za kitamaduni na kujumuisha aina mpya za sanaa.” alisema Naibu Rais.
Aliangazia umuhimu wa utamaduni katika maendeleo endelevu akitambua jukumu lake katika kuhimiza ujumuishaji katika jamii, ustahimilivu na ubunifu.
“Utamaduni wetu ndio msingi wa kujenga utajiri wetu.” aliongeza Kindiki huku akiangazia maudhui ya mwaka huu ya tamasha hilo ambayo ni “Utamaduni Wetu ni Nguzo ya Utajiri Wetu”.
Naibu huyo wa Rais alisisitiza kuhusu uwezo wa kiuchumi uliopo kwenye tasnia ya utamaduni na ubunifu inayochangia asilimia 5 ya pato jumla la taifa na uwezo wake wa kutoa nafasi za ajira kwa vijana.
Jambo lingine aliloangazia Kindiki ni jukumu la utalii wa utamaduni katika kutanua sekta ya utalii nchini akitaja hafla kama tamasha hilo la kitaifa la mashindano ya muziki ambalo linaweza kuvutia wageni.
Alimalizia kwa kusema kwamba serikali imejitolea kuunga mkono sekta za utamaduni na ubunifu.