Naibu Rais Rigathi Gachagua aliondoka hapa nchini Jumanne usiku, kuelekea Afrika Kusini kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwa rais wa taifa hilo Cyril Ramaphosa.
Ramaphosa ataapishwa leo Jumatano Jijini Pretoria, baada ya kuchaguliwa tena kuongoza taifa hilo, katika uchaguzi mkuu uliopita.
Naibu huyo wa Rais anamwakilisha Rais William Ruto katika hafla hiyo, ambako anatarajiwa kuwasilisha ujumbe wa Rais Ruto wa kumpogeza Ramaphosa na raia wa Afrika Kusini.
Chama cha ANC kinachoongozwa na Rais Cyril Ramaphosa, kilipoteza wingi wa wabunge kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30, katika uchaguzi wa mwezi uliopita.
Katika uchaguzi huo, ANC ilipata 40% ya kura, hatua iliyosababisha chama hicho kushirikiana na vyama vingine vya kisiasa ili kubuni serikali.