Naibu Gavana wa Homa Bay Joseph Oyugi Magwanga ajiuzulu

Tom Mathinji
1 Min Read

Joseph Oyugi Magwanga amejiuzulu wadhifa wa Naibu Gavana wa kaunti ya Homa Bay, akidai anahangaishwa katika utekelezaji majukumu yake.

Magwanga, ambaye alichaguliwa pamoja na Gavana Gladys Wanga katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2022, alisema ameshindwa kutoa huduma zake kutokana na vikwazo vilivyowekwa kwenye afisi yake.

Kulingana na Magwanga, afisi yake ilifungwa Mwezi Disemba mwaka jana huku akipokonywa gari lake rasmi na lingine likikosa kuwekwa mafuta.

Akiwahutubia wanahabari siku ya Alhamisi katika eneo la Oyugis, Kasipul, Magwanga alisema mazingira ya utendakazi hayamruhusu kutekeleza majukumu yake kikamilifu, hatua iliyomsababisha kujiuzulu badala ya kupokea mishahara bila kutoa huduma zake.

Aidha Magwanga alimlaumu Gavana Wanga kwa kutoheshimu hatua yake ya kutowania wadhifa wa Ugavana na kikubali kuwa mgombea mwenza.

Inaaminika kuwa aliyekuwa kiongozi wa chama cha ODM hayati Raila Odinga alimshawishi Magwanga kutowania Ugavana na badala yake kuwa Naibu Gavana wa Homa Bay.

Share This Article