Mamlaka ya Kupambana na Matumizi ya Dawa za Kulevya na Pombe Haramu nchini, NACADA limetakiwa kuimarisha juhudi za kupambana na matumizi ya pombe na dawa za kulevya nchini.
Wito huo umetolewa na Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo wakati akizindua mpango wa mkakati wa NACADA wa mwaka 2023-2027.
Dkt. Omollo alisifia mpango huo akisema una hatua madhubuti zinazolenga siyo tu kuongeza kiwango cha mafanikio yaliyopatikana katika vita dhidi ya matumizi ya pombe na dawa za kulevya nchini lakini pia namna ya kuimarisha kasi ya vita dhidi ya matumizi ya bidhaa hizo.
Mathalan, alisema mwaka huu pekee, serikali ilifanikiwa kufanya uvamizi 61,769 ambapo lita 342,088 za chang’aa na lita 2,553 za kangara zilinaswa. Aidha, lita 70,743 za pombe bandia zilinaswa na maduka 15,538 ya kuuza pombe na 381 ya kuuza shisha kufungwa. Kilo 6,047 za bangi pia zilinaswa na jumla ya watu 29,898 kukamatwa.
Dkt. Omollo alisema maeneo yaliyoathiriwa zaidi na matumizi ya pombe haramu na dawa za kulevya ni Bonde la Ufa, Nyanza, Magharibi, Kati na Nairobi.
Aliongeza kuwa kwa sasa, pombe ndio bidhaa inayotumiwa vibaya zaidi nchini huku vijana na taasisi za elimu zikiathirika mno.
Kulingana na takwimu za NACADA, karibu asilimia 40 ya watu wanaokunywa pombe humu nchini ni vijana huku mmoja katika kila Wakenya 7 wenye umri wa miaka 25-35 ambao idadi yao ni 1,137,288 wakiwa wanywaji wa pombe. Zaidi ya nusu ya idadi hiyo ambayo ni watu 596,336 ni waraibu wa pombe.