Mamlaka ya Kupambana na Pombe na Mihadarati humu nchini (NACADA) na maafisa wa polisi kutoka kitengo cha kukabiliana na mihadarati (ANU), wamenasa misokoto ya bangi 628 na lita 21 na nusu za pombe haramu ya chang’aa eneo la Pandipieri katika kaunti ya Migori.
Bangi hiyo ilikuwa imepakiwa katika magunia mawili na nyingine ndani ya beseni huku pia rununu mbili zikipatikana.
Baada ya kufanya msako zaidi katika jumba hilo, maafisa hao walipata makasha mengine 40, misokoto 230 ya bangi, lita moja na nusu za chang’aa, sigara ghushi, na mimea ya bangi iliyokaushwa chumbani humo.
Afisa Mkuu Mtendaji wa NACADA Dkt. Anthony Omerikwa amepongeza ushirikiano na juhudi za maafisa waliohusika kwenye msako huo.
“Ufanisi huu ni ishara ya nguvu na ushirikiano wa vyombo vyetu vya kiusalama katika jitihada za kumaliza matumizi ya mihadarati na pombe haramu. Tunajitolea kuilinda jamii dhidi ya athari za matumizi ya vileo,” aliahidi Omerikwa.
Bidhaa hizo zilizonaswa zitakaguliwa huku washukiwa waliokamatwa wakikabiliwa kisheria.
Omerikwa aliwaomba wananchi kuwa katika mstari wa mbele kupiga vita matumizi ya mihadarati na dawa za kulevya chini.