NACADA yanasa bangi ya thamani ya milioni moja Kitui

Maafisa wa NACADA walitekeleza operesheni ya pamoja mapema Alhamisi, wakilenga makazi ya mshukiwa pamoja na biashara zake.

Marion Bosire
2 Min Read

Maafisa wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kukabiliana na Matumizi ya Pombe na Mihadarati, NACADA, walitekeleza operesheni kubwa dhidi ya biashara ya dawa za kulevya katika Kaunti ya Kitui na kunasa bangi ya thamani ya shilingi milioni moja.

Mshukiwa anayesemekana kuwa mfanyabiashara mkubwa wa dawa hizo alitiwa mbaroni, kufuatia uvamizi uliofanywa alfajiri na maafisa hao wa NACADA.

Maafisa kutoka makao makuu ya NACADA jijini Nairobi walitekeleza operesheni ya pamoja mapema Alhamisi, wakilenga makazi ya mshukiwa pamoja na biashara zake.

Msako huo ulisababisha kupatikana kwa vijiti zaidi ya 5,600 vya bangi vilivyo tayari kutumika, vifaa vitatu vya kufungia bangi, bangi, mifuko ya plastiki, mizani na karatasi za kufungia bangi.

Akizungumza baada ya operesheni hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa NACADA, Dkt. Anthony Omerikwa, alithibitisha kuwa mamlaka hiyo ilikuwa ikifuatilia mshukiwa kwa wiki kadhaa kabla ya kumkamata.

“Operesheni ya leo inaonyesha dhamira thabiti ya NACADA kulinda jamii, hasa wakati huu shule zimefungwa na watoto wako nyumbani kwa likizo,” alisema Dkt. Omerikwa.

Aliongeza kwamba kama mamlaka, hawawezi kuruhusu wauzaji wa dawa za kulevya kuwavizia vijana wakati huu wako mbali na mazingira ya nidhamu ya shule.

Mkurugenzi huyo pia alipongeza wananchi kwa ushirikiano wao unaoendelea katika vita dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya. Mshukiwa kwa sasa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kitui akisubiri kufikishwa mahakamani.

Kukamatwa huku ni sehemu ya msururu wa oparesheni kali zinazofanywa na mamlaka hiyo kufuatia wito mpya wa Rais William Ruto wa kuongeza juhudi katika mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya nchini.

Mshukiwa amehamishiwa katika kituo cha polisi cha JKIA akisubiri kushtakiwa kwa makosa ya biashara haramu na umiliki wa dawa za kulevya.

Wananchi wote wenye taarifa kuhusu biashara ya dawa za kulevya katika maeneo yao wamehimizwa kutoa taarifa kwa NACADA au kituo cha polisi kilicho karibu nao.

Share This Article