NACADA: Uraibu wa mihadarati katika Vyuo Vikuu umeongezeka

Tom Mathinji
2 Min Read
Uraibu wa Mihadarati katika Vyuo Vikuu waongezeka.

Ripoti ya hivi punde ya Halmashauri ya kitaifa ya kukabiliana na uraibu wa Pombe na Mihadarati (NACADA), imedokeza ongezeko la utumizi wa mihadarati miongoni mwa vijana katika taasisi za elimu ya juu.

Kulingana na ripoti hiyo iliyozinduliwa leo Alhamisi kuhusu uraibu wa pombe na mihadarati katika vyuo vikuu vya hapa nchini, asilimia 45.6 ya wanafunzi wametumia mihadarati angalau mara moja katika maisha yao.

La kutamausha zaidi ni kwamba, asilimia 26.6 ya wanafunzi katika vyuo vikuu vya umma na vile vya kibinafsi, kwa sasa wanatumia mihadarati kama vile pombe, tumbako, bangi na miraa pamoja na matumizi ya dawa kama vile  methamphetamine na codeine syrup,.

Utafiti huo kulingana na NACADA, ulifanywa katika vyuo vikuu 17 za umma na kibinafsi katika maeneo ya Nairobi, Pwani, Nyanza, Magharibi, Kati , Mashariki, Kaskazini Mashariki na Rift Valley, ambapo wanafunzi 15,678 walihojiwa.

Aidha utafiti huo ulidokeza kuwa wanafunzi wengi walitumia pombe zaidi, utumizi wake ukiwa asilimia 87.3, huku mwanafunzi mmoja kati ya tano akiwa ametumia pombe katika muda wa mwezi mmoja uliopita.

Sigara ni ya pili kwa utumizi ikiwa na asilimia 64.4, Shisha asilimia 41.2, sigara aina ya vape asilimia 31.06 nicotine asilimia 30.7, kuber asilimia 23.0 na tumbaku ikawa na asilimia 22.1.

Katika ripoti hiyo, marafiki walitambuliwa kuwa wanaofanikisha upatikanaji wa mihadarati kwa wanafunzi, wakiwa na asilimia 66.4, mikahawa ikiwa ya pili, baa na maeneo jirani yakiwa ya mwisho kwa asilimia 56.

Ununuzi kupitia mtandaoni pia umetajwa kufanikisha upatikanaji wa mihadarati kwa asilimia 39.4 .

La kushangaza zaidi katika ripoti hiyo ni kwamba asilimia 70 ya vijana wa kizazi cha Gen Z walioshiriki maandamano mwaka jana, walikiri walitumia bangi kwa mara kwanza zaidi wakati wa maandamano hayo.

Ripoti hiyo iliashiria changamoto kuu za kiafya zinazotokana na uraibu wa mihadarati ikiwa ni ongezeko la uraibu na magonjwa ya akili.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article