Mwili wapatikana kwenye gari la mwanamuziki D4vd

Marion Bosire
2 Min Read
Mwanamuziki D4vd

Maafisa wa polisi huko Los Angeles nchini Marekani wanachunguza kisa ambapo mwili wa binadamu ulipatikana ndani ya gari la mwanamuziki wa umri wa miaka 20, D4vd ambaye jina lake halisi ni David Anthony Burke.

Mwili huo uliokuwa ukioza uligunduliwa kwenye gari hilo aina ya Tesla lililokuwa katika kituo cha maegesho ya magari yaliyotwaliwa huko Hollywood Calif Jumatatu jioni kulingana na saa za Marekani.

Uchunguzi wa mwanzo ulionyesha kwamba gari hilo limesajiliwa kwa jina la mwanamuziki huyo ambaye kwa sasa anaendeleza ziara ya kikazi na alipangiwa kutumbuiza huko Minneapolis Jumanne usiku kwa saa za Marekani.

Wafanyakazi wa kituo hicho cha maegesho ya magari yaliyotwaliwa walihisi uvundo mkali ukitoka kwenye gari hilo na wakajulisha maafisa wa polisi waliofika katika eneo la tukio.

Kufikia sasa mwili huo bado haujatambuliwa na hata jinsia ya mwendazake bado haijabainika kutokana na kiwango cha kuoza kwa mwili huo.

Gari hilo lililoundwa mwaka 2023 liliburutwa na kupelekwa kwenye kituo hicho cha maegesho baada ya kutelekezwa katika eneo la Hollywood Hills kwa zaidi ya siku tano.

Mwili huo unaaminika kuwa kwenye gari hilo kwa siku hizo tano na siku nyingine kadhaa katika kituo hicho cha maegesho ya magari ndiposa umeoza.

Mwanamuziki huyo hata hivyo aliendelea na tumbuizo lake katika eneo la burudani la The Fillmore huko Minneapolis jinsi ilivyokuwa imepangwa.

Website |  + posts
Share This Article