Mwili wa Raila wapokelewa uwanjani JKIA

Hayati Raila aliyefariki akiwa na umri wa miaka 80, atapumzishwa siku ya Jumapili nyumbani kwake Bondo.

Dismas Otuke
1 Min Read

Mwili wa kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga umewasilishwa nchini mapema leo kutoka nchini India alikofariki jana Jumatano kutokana na mshtuko wa moyo.

Rais William Ruto na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta wameupokea mwili wa BABA Raila katika uwanja wa JKIA.

Kama njia ya kutoa heshima kwa BABA, kampuni ya Kenya Airways imebadilisha jina la ndege iliyoubeba mwili wa marehemu na iliitwa nambari ya usajili RAO001 punde baada ya kuingia katika anga ya Kenya.

Ujumbe wa maafisa wakuu serikalini ukiongozwa na kinara wa mawaziri Musalia Mudavadi ulisafirisha mwili wa marehemu Raila kwa kutumia ndege ya shirika la ndege nchini Kenya Airways.

Mwili wa kiongozi huyo utapelekwa katika makafani ya Lee na baadaye kupelekwa katika majengo ya Bunge kuanzia saa sita leo Adhuhuri.

Maombi ya kitaifa kwa heshima za Baba yataandaliwa kesho Ijumaa katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo ambapo wananchi watautazama mwili wake kabla ya kusafirishwa kwa ndege hadi nyumbani kwake Bondo siku ya Jumamosi.

Hayati Raila aliyefariki akiwa na umri wa miaka 80 atapumzishwa siku ya Jumapili.

Rais William Ruto alitangaza maombolezi ya kitaifa ya siku saba kuanzia jana kumuenzi Baba.

Website |  + posts
Share This Article