Mwigizaji wa muda mrefu wa filamu za Nigeria almaarufu Nollywood mama Nkechi Nweje amefariki, baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Kifo cha mama Nkechi kilithibtishwa Jumamosi Machi 22, 2025 na mtayarishaji filamu kwa jina Stanley Ajemba, ambaye anafahamika sana kama Stanley Ontop, kupitia Instagram.
“Nollywood inalia tumepoteza mmoja wa waigizaji wetu bora Nkechi Nweje baada ya kuugua kwa muda mfupi.” aliandika Stanley chini ya picha ya Nkechi aliyochapisha.
Aliendelea kuelezea kwamba alishindwa kuchapisha habari hizo kwa muda kwa sababu hakuamini, “Ilikuwa kama ndoto kwangu” aliongeza.
“Lala salama mama, rafiki yangu wa dhati, alikuwa akinipigia simu kila mara kunishauri.” aliandika mwandaaji huyo wa filamu.
Mwigizaji mwingine wa Nollywood mama Rita Edochie, alichapisha picha ya mshumaa kwenye Instagram na kuandika, “Hii dunia kweli sio kwetu”.
Waigizaji wengine wengi wa Nollywood nao wamemwomboleza mama huyo ambaye alifariki kutokana na ugonjwa ambao haukuwekwa wazi.
Mama Chinyere Wilfred alichapisha picha za mwendazake na kuandika, “Ni vigumu kusema kwaheri NK”.
Nweje alikuwa na talanta ya kipekee katika uigizaji ambapo mara nyingi alikuwa anapatiwa majukumu ya kuigiza kama mama mwenye mapenzi kwa wanawe.
Ameigiza kwenye filamu zaidi ya 100 za Nollywood na urithi wake katika tasnia ya uigizaji kamwe hautasahaulika.
Nkechi Nweje ameacha mume wake Daktari Azuibuike Nweje na watoto sita.