Mwigizaji mkongwe O Yeong Su ahukumiwa kifungo gerezani

Su anadaiwa kumkumbatia kwa lazima na kumbusu mwanamke mmoja wa umri mdogo ambaye alikuwa mwanachama wa kundi lake la waigizaji, karibu na nyumbani kwake.

Marion Bosire
2 Min Read
O Yeong-su,

O Yeong Su wa umri wa miaka 80 ambaye ni mwigizaji kutoke Korea Kusini, amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja gerezani.

Su ambaye alijipatia umaarufu ulimwenguni kufuatia uhusika wake katika filamu ya Squid Game alikoigiza kama Oh Il Nam, alipokea hukumu hiyo kutokana na kisa kilichotokea mwaka 2017.

Kulingana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani, Su anadaiwa kumkumbatia kwa lazima na kumbusu mwanamke mmoja wa umri mdogo ambaye alikuwa mwanachama wa kundi lake la waigizaji, karibu na nyumbani kwake.

Mwanamke huyo aliambia mahakama kwamba mzee huyo alimdhulumu kingono mara mbili.

Katika kikao cha mwisho cha kusikiliza kesi hiyo, waendesha mashtaka walisema kwamba vitendo vya mzee huyo vilidhihirisha matumizi mabaya ya mamlaka ya mwigizaji tajika na mkongwe dhidi ya mwenzake mdogo.

Waliendelea kusema kwamba O Yeong Su ni mtu ambaye ana ushawishi mkubwa katika tasnia ya uigizaji ambaye alitumia nafasi yake kudhulumu mtu ambaye ana kiwango kidogo cha uwezo na ushawishi.

Hata baada ya kupatikana na hatia na kuhukumiwa, O Yeong Su ameshikilia kwamba hana makosa hata katika hotuba aliyotoa mahakamani.

“Ninaaibika kusimama katika mahakama hii kwa umri huu. Iwapo maneno yangu na matendo yalikuwa mabaya, nitakubali matokeo.” alisema mzee huyo.

Awali alikuwa amepatiwa hukumu ya kifungo cha miezi minane gerezani na kifungo cha nje cha miaka miwili lakini baada ya kikao cha rufaa, hukumu hiyo ilibadilishwa na kuwa mwaka mmoja gerezani.

Website |  + posts
Share This Article