Mwenyekiti wa AU asema Afrika inazingatia uundaji wa nafasi za ajira

Marion Bosire
1 Min Read

Mwenyekiti wa Kundi la Marais wa Mataifa ya Umoja wa Afrika, AU Azali Assoumani amesema Bara la Afrika linazingatia uundaji wa nafasi za ajira pamoja na masuala ya dijitali.

Akizungumza kwenye kongamano la pili la ushirikiano kati ya Urusi na Afrika jijini St. Petersburg, Assoumani alisema pia kwamba Afrika imejitolea kushirikiana na Urusi.

Kiongozi huyo wa nchi ya Comoros alisema nyanja ambazo bara hili linashirikiana na Urusi ni kama vile kilimo, nishati, nafasi za ajira kwa vijana na teknolojia ya kisasa.

Alisema Afrika inatekeleza juhudi za kuhakikisha amani na usalama na inaamini katika ushirikiano wa heshima na wenye manufaa.

Alikashifu matukio ya nchini Niger akisema Umoja wa Afrika unataka Rais Mohamed Bazoum na familia yake waachiliwe huru.

Kuhusu makubaliano ya nafaka, Rais Assoumani alisema Urusi imekuwa muhimu katika kukabiliana na njaa barani humu.

Kongamano la pili la ushirikiano kati ya Urusi na Afrika lilianza leo Alhamisi nchini Urusi na litakamilika kesho.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni anahudhuria huku Rais wa Kenya William Ruto akiamua kutohudhuria na badala yake kuwakilishwa na Umoja wa Afrika.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *