Mwanahabari mkongwe na mfanyabiashara wa Uganda Andrew Mwenda ametangaza mipango ya kumhoji mkuu wa jeshi la Uganda Jenerali Muhoozi Kainerugaba katika kipindi cha mitandaoni.
Katika taarifa aliyochapisha kwenye mtandao wa X, Jumamosi, Januari 11, 2025, Mwenda, ambaye ni msemaji wa kundi la wazalendo wa Uganda ambalo Muhoozi ni mwenyekiti wake alielezea hatua ya Muhoozi kufuta akaunti yake ya X.
Kulingana naye, kundi fulani la wanajeshi wa Uganda, lilisisitiza kwamba Muhoozi ajiondoe kwenye mtandao wa X hadi pale ambapo mageuzi katika jeshi yatakapokamilika.
Mwenda alisema kama mwanajeshi mtaalamu, mzalendo, mpenda Afrika na mtu anayependa jeshi la Uganda, Muhoozi alikubali ombi la wanajeshi hao.
Aliendelea kusema kwamba mkuu huyo wa majeshi ya Uganda atazindua kipindi cha mitandaoni ambacho kitaandaliwa mara moja kila mwezi ambapo ataangazia historia na matukio ya sasa katika kiwango cha kimkakati.
Kipindi hicho cha mitandaoni kitafahamika kama ‘Muhoozi-Mwenda Dialogue’ na makala ya kwanza yanatarajiwa kwenye mtandao wa YouTube Januari 28.
Mwenda alialika vituo vya televisheni nchini humo kuwania haki za kupeperusha kipindi hicho.