Mwelekezi wa filamu Dimeji Ajibola afariki

Marion Bosire
1 Min Read

Dimeji Ajibola ambaye ni mwelekezi wa filamu za Nollywood nchini Nigeria amefariki.

Kando na kuelekeza filamu, Ajibola, alikuwa pia anahusika na uhariri wa filamu kama ile maarufu ya “Shanty Town”.

Kifo chake kilitangazwa na wenzake katika tasnia ya filamu nchini Nigeria kama vile Bolanle Ninalowo, Uzee Usman na Chinenye Nworah jana Jumapili ila kilichosababisha kifo hicho hakikufichuliwa.

Nworah alimtakia Ajibola ambaye alimrejelea kama ndugu usiku mwema milele huku akikiri kwamba hajui cha kuandika anapomwomboleza.

Ninalowo naye alikiri mapenzi aliyonayo kwa mwendazake akisema atamkosa sana. Aliitakia familia ya Ajibola faraja wakati huu mgumu.

Ajibola amefanya kazi katika tasnia ya filamu nchini Nigeria kwa zaidi ya miaka 18 ambapo alianza kama muunda filamu zu video za vibonzo.

Alipokea mafunzo kuhusu uundaji wa filamu katika taasisi ya ‘New York Film Academy’ akapokea mafunzo ya kuunda filamu za vibonzo kwenye ‘Animation Mentor’ huko San Francisco nchini Marekani na yaa uundaji wa picha kwenye tarakilishi katika taasisi ya mitandaoni iitwayo ‘VFXLearning’.

Dimeji alikuwa anamiliki studio za Flipsyde ambapopia alikuwa anahudumu kama mkurugenzi wa masuala ya kiufundi.

Kando na filamu, alihusika kwenye maandalizi ya matangazo ya kibiasgara ya kampuni za MTN na Coca-Cola.

Share This Article